Njia nne ambazo dhambi zinaweza kumwingia mtu
Four ways through which sins may invade a person
Kwa kuwa chanzo cha uovu wa uzinzi ni kuona, Allah ~ ameamuru Waislamu wapunguze kutazama; kwani uovu huanza kwa kutazama, kisha hisia za tamaa, kisha kusogea karibu, na mwishowe kutenda kitendo cha dhambi. (1) Kutazama kitu kisichohalali ndiyo njia kuu ya kuzalisha tamaa, na hivyo yeyote anayejizuia nacho, kwa kweli amehifadhi usafi wake. Mtume ﷺ amesema: "Usitazame mara ya pili, kwa sababu ingawa wewe huna lawama kwa mara ya kwanza, huna haki kwa mara ya pili."3 Mtume ﷺ pia amesema: "Kutazama ni mojawapo ya mishale yenye sumu ya Iblis (Shetani), hivyo yeyote anayeshusha macho yake asitazame uzuri wa mwanamke, Allah atamjalia ibada ambayo ataonja utamu wake."4 Mtume ﷺ pia amesema: "Angalieni! Epukeni kukaa njiani." Wakasema: "Ee Mjumbe wa Allah! Hatuwezi kuacha kukaa (njiani) kwani hapa ndipo mahali petu pa kupiga stori." Mtume ﷺ akajibu: "Ikiwa lazima mkae, basi mpeni barabara haki yake." Wakauliza: "Haki ya barabara ni ipi, Ee Mjumbe wa Allah?" Akajibu: "Kupunguza kutazama, kujizuia kuwadhuru wengine, kujibu salamu, kuamrisha mema na kukataza maovu."5 Kutazama kuko nyuma ya baadhi ya majanga makuu yanayowapata wanadamu. Kwa hakika, kutazama huzalisha tamaa; tamaa huzalisha mawazo; mawazo huzalisha shauku; shauku huzalisha nguvu ya nia inayogeuka kuwa azma thabiti, na mwishowe kuwa kitendo, mradi tu hakuna kizuizi. Katika muktadha huu, imesemwa: "Subira katika kupunguza kutazama ni rahisi (kuivumilia) kuliko subira na maumivu ya matokeo ya kutazama huko." (2) Matamanio na mielekeo ndiyo chanzo cha mema na maovu, na ni kutoka kwake ndipo hutokea nia na azma. Kwa hiyo, atakayedhibiti matamanio yake amejidhibiti kweli; na atakayejisalimisha kwa matamanio yake, atazidiwa nayo; lakini atakayeyadharau matakwa yake, yatamwongoza kwenye uharibifu wa nafsi yake. Matamanio huendelea kukaribia moyo hadi yakageuka kuwa matakwa, kama alivyosema Allah ~: (.. kama mwangaza wa mbali jangwani. Mwenye kiu huudhania kuwa ni maji mpaka akiufikia, hukuta si kitu; lakini humkuta Allah pale, Ambaye atamlipa haki yake. Allah ni Mwepesi wa kuhesabu) 1 Watu wanaodharauliwa zaidi, kwa kuzingatia azma yao, ni wale wanaogeuza mambo halisi kuwa matakwa ya uongo, na kuyashikilia katika maisha yao duni. Matakwa haya ya uongo ni hatari kwa mwanadamu, kwani huzaa hali ya uvivu na kutojali, na huleta hisia za kupuuza, majuto na kujuta. Mtamanio anapokosa mwingiliano wa ukweli ndani ya mwili wake, huchora picha yake moyoni mwake, na hivyo huridhika na picha za kufikirika zinazoletwa na mawazo yake mwenyewe, ambazo kamwe hazimletei kuridhika halisi maishani. Mfano wake ni kama wa mtu aliye na njaa na kiu, anayejiwazia picha za chakula na kinywaji akilini, bila kuwa na chakula wala kinywaji cha kumtuliza njaa na kiu yake. Kukubali hali ya namna hii huonyesha kiwango cha chini cha kujiheshimu na pia ni aibu; kwa sababu heshima na usafi wa nafsi unategemea kukataa matamanio yoyote yasiyo ya kweli au ndoto. Matamanio ya mwanadamu yanaweza kugawanywa katika makundi manne: Matamanio ambayo kwayo mwanadamu hupata manufaa ya kidunia, matamanio ambayo kwayo huondoa matatizo yake ya kidunia, matamanio ambayo kwayo hupata manufaa Akhera, na matamanio ambayo kwayo huondoa madhara yoyote Akhera. Mtu mwenye akili hatasita kupendelea matamanio yatakayomletea manufaa Akhera, kwa kutafuta Radhi za Mola wake. Mawazo na matamanio kama haya yamepangwa kulingana na vipaumbele vyake: Kwanza, kutafakari Wahyi na kuelewa maana yake. Allah ~ hakuuteremsha ili usomwe tu. Badala yake, kusomwa kwake ni njia tu ya kumwezesha mtu kutafakari maudhui yake. Mwanazuoni mmoja wa zamani alisema: "Qur'ani iliteremshwa ili itekelezwe; basi geuza usomaji wake kuwa vitendo!" Pili, kutafakari Ishara za Allah na kuzitumia kama ushahidi wa kuthibitisha Majina ya Allah, Sifa Zake, Hekima Yake, Wema Wake na Ukarimu Wake, kwa kuwa Allah ~ amewahimiza Waja Wake kutafakari Ishara Zake na kuzielewa. Tatu, kufikiria Wema wa Allah, Msamaha Wake, Rehema Yake, Subira Yake, na jinsi anavyowamiminia Waja Wake Baraka Zake. Aina hizi tatu za tafakuri huchota moyoni: elimu, mapenzi na khofu ya Allah, ambavyo vinaweza kuimarishwa kwa kumkumbuka Allah ~. Nne, kufikiria kasoro za nafsi na za matendo ya mtu. Fikra hii ina athari kubwa yenye manufaa, kwani huivunja nafsi inayoamrisha uovu, na kumruhusu moyo wa mtu kuishi katika ulimwengu wenye utulivu. Tano, kufikiria wajibu wa wakati na kazi yake, na kuelekeza wasiwasi wote kuuzunguka, ili kuepuka kupoteza hata sehemu moja yake. Kwa hakika, manufaa yote hutokana na wakati, na wakati uliopotezwa hauwezi kurudishwa. Mwanazuoni Shafi'i alisema: "Nimeshirikiana na watu wa Sufi na sikupata faida kutoka kwao isipokuwa maneno mawili: kwanza, kauli yao: 'Wakati ni upanga; usipoukata, utakukata.' Pili, 'Usipojishughulisha na haki, itakujaza batili.' Muda wa mtu ni kwa hakika maisha yake yote; ni njia inayomwongoza kwenye maisha yake ya milele yaliyobarikiwa (Peponi), au njia ya maisha yake ya milele ya adhabu (Motoni). Hupita kwa kasi kuliko mawingu yanavyosogea." Maisha halisi ya mtu ni kiasi chochote anachotumia katika kumtii Allah ~, na kila kitu kingine hakiwezi kuhesabiwa kuwa maisha yake; hata kama ameshaishi muda huo, maisha yake yanaweza kulinganishwa na yale ya wanyama. Hata mtu anayeswali Sala haipati kutoka kwenye Sala yake isipokuwa kile anachokikumbuka kati yake; kwa hiyo maisha ya binadamu ni yale tu yaliyotumika katika kumtii Allah ~, na kila kitu kingine si chochote ila minong'ono ya shetani na matamanio ya uongo. Mnapaswa kujua kwamba tamaa yenyewe haimdhuru mtu; kinachodhuru ni kushirikiana nayo au kuitikia. Tamaa ni kama mpita njia; ukiipuuza, itaondoka; lakini ukiikaribisha ndani, itakuroga kwa maneno yake ya udanganyifu. Allah ~ amemweka mtu nafsi mbili: nafsi inayoamuru na nafsi tulivu, na hizi zinapingana; kile kinachopendeza kwa moja ni kizito kwa nyingine, na kile kinachomridhisha mmoja kinamtesa mwingine. Malaika yuko upande wa kulia wa moyo, na shetani yuko upande wa kushoto wake. Kuna vita endelevu, hadi nafsi ikamilishe maisha yake duniani. Uongo wote uko upande wa shetani na nafsi inayoamuru maovu; ukweli wote unabaki upande wa Malaika na akili tulivu. Vita hii endelevu imeandikwa, na ushindi unapatikana kwa subira ya mtu. Yeyote anayevumilia, akasubiri kwa subira na kumcha Allah atakuwa na mwisho mwema duniani na Akhera. Allah ~ ameamua kwamba mwisho uliobarikiwa ni kwa wacha Mungu. (3) Maneno yanapaswa kuhifadhiwa na kutumiwa kwa yale tu yenye manufaa. Mtu anapaswa kusema yale tu yanayofaa kwa Dini yake. Kabla ya kutamka neno, mtu anapaswa kufikiri mara mbili, kuhusu kama ni la manufaa kwa Dini yake au la; ikiwa hakuna faida katika kulisema, ajizuie kulitamka; lakini ikiwa lina faida yoyote, asipoteze nafasi ya kulisema. Ikiwa mtu anataka kutoa ushahidi kuhusu yaliyomo ndani ya nyoyo (za wengine), basi ni lazima azingatie maneno yao. Kwa kweli, ulimi hufichua hali ya moyo, iwe mwenyewe anapenda au hapendi! Yahya bin Mu'adh alisema: "Nyoyo ni kama vyungu vya kupikia vyenye vilivyomo vikichemka, na ndimi ni vijiko vyake. Mtu anapozungumza, ulimi wake huchota kilichomo moyoni mwake; kitamu au chungu." Anas bin Malik ~ alisimulia kwamba Mtume ﷺ alisema: "Imani ya mtu haiwi sawa mpaka moyo wake uwe sawa; na moyo wake hauwi sawa mpaka ulimi wake uwe sawa." Abdullah bin Mas'ud ~ alisimulia kwamba Mtume ﷺ alisema: "Naapa kwa Yule ambaye roho yangu iko mikononi mwake, mtu si Muislamu mpaka moyo wake na ulimi wake viwe vimenyenyekea." Mtume ﷺ aliulizwa kuhusu mambo yanayowaingiza watu wengi Motoni, naye ﷺ akajibu: "Mdomo na sehemu za siri." Mu'adh alimuuliza Mtume ﷺ kuhusu tendo ambalo lingemwingiza Peponi na kumweka mbali na Moto. Mtume ﷺ akamjulisha kwamba msingi wa jambo ni Uislamu, nguzo zake ni Sala, na kilele chake ni kupigania Dini ya Allah (Jihadi). Kisha akauliza: "Je, nikujulishe kilicho chini ya haya yote?" Mu'adh akajibu: "Hakika, ee Mjumbe wa Allah." Mtume ﷺ akashika ulimi wake na kusema: "Uzuie hili." Mu'adh akasema: "Je, tutawajibishwa kwa yale tunayosema?" Akajibu: "Mama yako akupoteze! Je, watu hawatatupwa kifudifudi Motoni ila kwa sababu ya mavuno ya ndimi zao?" Jambo la ajabu ni kwamba kuna hali ambapo mtu anaweza kupata urahisi wa kujizuia na mambo ya Haramu kama vile kudhulumu, zinaa, wizi, kunywa pombe au kutazama yasiyo halali, lakini anaona ni vigumu kuudhibiti ulimi wake, na unamwona akitamka maneno yanayoleta Laana ya Allah ~ juu yake! Hadithi ya Jundub bin Abdullah ~ inaeleza hali kama hii. Alisema: "Nabii ﷺ alisema kwamba mtu mmoja alisema: 'Allah hatamsamehe mtu fulani.' Ndipo Allah ~ akasema: 'Ni nani huyu anayeapa juu Yangu kwamba sitamsamehe fulani? Nimemsamehe fulani na nimefuta amali zako (amali za yule aliyeapa kwamba Allah hatamsamehe mtu huyo).'" Kwa hiyo mtu huyo mcha Mungu aliyemwabudu Allah ~ maisha yake yote, amali zake zilifutwa kwa neno moja tu alilolitamka! Akisimulia Hadithi hiyo hiyo, Abu Hurayrah ~ alisema: "Mtu yule alitamka neno moja lililoharibu maisha yake duniani na Akhera!" Abu Hurayrah ~ alisema: "Nabii ﷺ alisema: 'Mja (wa Allah) anaweza kutamka neno linalompendeza Allah bila kulipa umuhimu mkubwa; kwa sababu hiyo Allah ~ atamwinua kwa daraja (za thawabu); na mja (wa Allah) anaweza kutamka neno (bila kujali) linalomchukiza Allah bila kufikiria uzito wake; na kwa sababu hiyo atatupwa Motoni.'" Bilal bin Al-Harith ~ alisimulia kwamba Nabii ﷺ alisema: "Mtu husema neno jema bila kutambua thamani yake; ambalo Allah humwandikia kwa Radhi Yake mpaka siku atakapokutana Naye. Mtu pia husema neno baya bila kutambua umuhimu wake, ambalo Allah humwandikia Ghadhabu Yake mpaka siku atakapokutana Naye." 'Alqamah alikuwa akisema: "Hadithi ya Bilal bin Al-Harith ilinizuia kusema maneno mengi!" Anas bin Malik ~ alisema: "Mmoja wa Maswahaba alipofariki, mtu mmoja alisema: 'Furahini kwa Pepo yake.' Lakini Nabii ﷺ akasema: 'Je, mnasema hivi hali ya kuwa hamjui kama labda alisema yasiyomhusu, au alikuwa bahili kwa kitu ambacho kisingemletea hasara?'" Abu Hurayrah ~ alisimulia kwamba Nabii ﷺ alisema: "Anayemwamini Allah na Siku ya Mwisho na aseme neno jema au anyamaze." 6 Abu Hurayrah ~ pia amesimulia kwamba Mtume ﷺ alisema: "Sehemu ya uzuri wa Uislamu wa mtu ni kuacha yale yasiyomhusu." 1 Sufyan bin Abdillah At-Thaqafi ~ alisema: "Nilisema: 'Ewe Mjumbe wa Allah, niambie jambo kuhusu Uislamu ambalo sitaweza kumuuliza mtu mwingine yeyote isipokuwa wewe'. Naye ﷺ akasema: "Sema: 'Ninamwamini Allah', kisha simama imara." Nikasema: 'Ewe Mjumbe wa Allah, ni jambo gani unaloogopa zaidi kwangu?' Akashika ulimi wake mwenyewe akasema: "Hili!" 2 Umm Habibah ,$,, mke wa Mtume ﷺ, ameripoti kwamba Mtume ﷺ alisema: "Kila neno analolisema mwana wa Adam linahesabiwa dhidi yake wala si kwa manufaa yake, isipokuwa: kuhimiza lililo jema, kukataza lililo baya, au kumtaja Allah." 3 Katika Hadithi nyingine, Mtume ﷺ alisema kwamba mtu anapoamka asubuhi, viungo vyote hujinyenyekeza mbele ya ulimi na kusema: "Mcha Allah kwa ajili yetu, kwa kuwa sisi tunakutegemea; ukiwa mnyoofu nasi tunakuwa wanyoofu, lakini ukiwa mpotovu nasi tunakuwa wapotovu." 4 Wanazuoni wametofautiana kuhusu kama kila kitu mtu anachokitamka kinaandikwa au ni kile tu kinachohusu mema na maovu, huku mtazamo wa kwanza ukipewa uzito zaidi, kwa sababu Allah ~ amesema: (Hatamki neno lolote isipokuwa kuna mlinzi tayari kulirekodi.)5 Kuna magonjwa mawili makubwa yanayohusiana na ulimi; mtu akiwa salama kutokana na moja, hayuko salama kutokana na jingine; nayo ni magonjwa ya "kusema" na ya "kunyamaza". Moja linaweza kuwa dhambi kubwa kuliko jingine; kwani mtu anayenyamazia ukweli ni "shetani bubu", aliyeasi amri ya Allah ~; ilhali mtu anayesema uongo ni "shetani msemaji", aliyeasi amri ya Allah ~. Watu wema ni wale wanaozuia ndimi zao kutamka uongo, lakini wanazilegeza kusema yale yenye manufaa kwao katika Akhera yao. Mtu anaweza kuja Siku ya Kiyama akiwa na matendo mema yenye ukubwa wa milima, lakini yakaharibiwa na ulimi wake; au mtu anaweza kuja akiwa na matendo mabaya yenye ukubwa wa milima, lakini akakuta kwamba ulimi wake uliyaharibu kwa kumkumbuka Allah mara kwa mara! (4) Hatua za miguu zinapaswa kuhifadhiwa kwa maana kwamba mtu lazima atumie miguu yake kumpeleka mahali ambapo atapata Thawabu za Allah, si Laana Yake. Kwa kuwa kuteleza kunahusiana na mguu pamoja na ulimi, vyote viwili vimetajwa katika Aya, kama Allah ~ alivyosema: ( Waja wema wa Mwingi wa Rehema (Allah) ni wale wanaotembea juu ya ardhi kwa unyenyekevu na utulivu, na wajinga wanapowasemesha (kwa maneno mabaya) hujibu kwa maneno laini ya upole. ) 6 Allah ~ aliwaelezea waja Wake waaminifu kwa unyoofu katika maneno yao na hatua zao.